Rais John Magufuli awabeba wawekezaji wa ndani

RAIS John Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kuwasaidia na kuwaunga mkono wawekezaji wote wa ndani, watakaoanzisha viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.

Pia amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha anatengeneza mazingira yatakayowapunguzia kwa kiasi kikubwa kodi wawekezaji wa ndani na kupandisha kodi zaidi kwa bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi.

Dk Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wa mwaka ulioandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa ajili ya utoaji wa Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora nchini.

Alisema Tanzania ni nchi yenye utajiri wa rasilimali, fursa ya masoko, nguvukazi na mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo kipaumbele kikubwa kitakuwa ni kuhakikisha wazalendo wanapata fursa ya kufungua viwanda kwa wingi na kutumia ipasavyo fursa hiyo.

“Mchango wetu Afrika kiuchumi duniani uko chini ya asilimia tano, sasa ili tuweze kufikia malengo ya kukua zaidi kiuchumi, Afrika hatuna budi kufanya mageuzi ya sekta ya viwanda,” alisisitiza.

Alisema endapo wafanyabiashara wa Tanzania watawekeza na kuanzisha viwanda nchini, watapata faida kubwa, wataongezea nchi mapato, kuingiza zaidi fedha za nje na kutengeneza ajira kwa wingi.

Alisema kuendelea kutegemea na kutoa kipaumbele kwa bidhaa za nje hakuna faida zaidi ya hasara kwa Watanzania kwani pamoja na bidhaa hizo wakati mwingine kuingizwa kwa njia za panya na kuwa feki au bandia, pia watengenezaji wake wako nje ya nchi.

Alisema kwa kuwa watengenezaji wake wako nje ya nchi, Tanzania haipati mapato zaidi ya ushuru wa kuingiza bidhaa hizo lakini pia ajira zinazotengenezwa zaidi ni kwa nchi ambazo bidhaa hizo zinatengenezwa.

Aliwataka Watanzania hasa watendaji kuondokana na tabia ya wivu kwa kuwanyima fursa wawekezaji wa ndani pindi wanapotaka kuwekeza na badala yake kupendelea na kuwaamini zaidi wawekezaji kutoka nje.

“Matokeo yake, tunakuwa na rasilimali nyingi lakini tunashindwa kuziboresha, wanakuja watu wa nje wanachukua mahindi yetu wanasaga na kuuza Sudan Kusini kwa bei ya juu, tuacheni hii dhambi ya wivu ya kunyima fursa pindi mmoja wetu akitaka kuwekeza sehemu…”

“…nimeshamwambia Waziri wangu Serikali hii ya Awamu ya Tano inatoa fursa mtu kuwekeza popote hata kama ni mzalendo, ukitaka kuwekeza kwenye mbolea, gesi, saruji, kilimo au mafuta ruksa,” alisisitiza.

Alisema kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili au ya tatu Afrika kwa ufugaji wa ng’ombe lakini cha kushangaza hakuna kiwanda cha kutengeneza viatu, mabegi wala mikanda. “Ng’ombe wetu hawa wanachukuliwa watu wanaenda kutengeneza bidhaa hizi wanazirudisha na kutuuzia kwa bei ya juu.”

Alisema uwekezaji katika sekta ya viwanda ukikua nchini hata wakulima wa pamba, korosho, kahawa na mazao mengine ya biashara watazalisha kwa wingi na kupata faida kwa kuwa watakuwa na soko la uhakika lakini pia viwanda hivyo vitatengeneza ajira na kuuza bidhaa hiyo kwa bei ambayo Watanzania wataimudu.

Alisema serikali yake imejipanga kuwaunga mkono wawekezaji wa kizalendo watakaoanzisha viwanda na nguvu kubwa imeelekezwa katika uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji utakaotumia kwa wingi malighafi zinazozalishwa nchini.

Dk Magufuli alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kupitia sekta hiyo ya viwanda ifikapo 2020 ichangie katika Pato la Taifa kwa asilimia 40 lakini pia ajira zitakazozalishwa kupitia viwanda pia zifikie asilimia 40.

“Naamini jambo hili linawezekana kwa sababu nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali zinazowezesha kujenga uchumi wa viwanda, tunayo ardhi ya kutosha, nguvu kazi, misitu, samaki kupitia uvuvi, soko la uhakika kwa kuwa tumezungukwa na nchi zisizo na maji,” alisema.

Aidha, alisema Tanzania ina fursa nzuri za uwekezaji kwa kuwa iko katika ushirikiano wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) hivyo kuwa na uwezekano wa soko la watu zaidi ya milioni 390.

Alisema nchi zote duniani zilizokuwa na hali mbaya ya uchumi ziliweza kuendelea baada ya kuwekeza zaidi nguvu zake katika sekta ya viwanda na sasa nchi hizo ndio zinazoongoza duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa.

Alitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni China, Korea Kusini, Thailand, Malaysia, Vietnam iliyochukua mbegu za korosho nchini na sasa ndio inayoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo na Mauritius inayoongoza duniani kwa uzalishaji sukari.

Rais aliwaahidi wawekezaji wa ndani kuwa serikali italinda viwanda vyote vya ndani kwa kuhakikisha inaondoa mazingira yote yanayoweza kusababisha vikose soko, vishindwe kuzalisha na kufa.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda nchini, alisema kubwa ya miundombinu tayari serikali inaifanyia kazi, na mwaka ujao wa fedha imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kisasa.

Aidha, alisema Tanzania iko katika mazungumzo ya mwisho na Zambia kwa ajili ya kuifanyia ukarabati reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) pamoja na kujipanga kuondoa kabisa kero ya umeme kupitia miradi mbalimbali ya umeme inayoendelezwa nchini.

Kuhusu suala la utitiri wa tozo kwa wawekezaji wa viwandani, Dk Magufuli alieleza kuwa serikali imeshaunda kamati ya kitaifa kwa ajili ya kuangalia mazingira ya tozo na endapo kutakuwa na tozo zisizo na tija zilizolenga kuwanufaisha wachache zitaondolewa.

“Ni kweli nchi yetu ina vikodi vingi hasa kwenye mazao kama vile kahawa, pamba na korosho, na ninafahamu kuna kodi nyingine ni kwa ajili ya kuliwa na baadhi ya watu, hizi nitaziondoa. Ndio maana wengine wananiita mkorofi lakini ninasimamia haki na si lingine,” alisema.

Waziri Mwijage alisema serikali imeanza kuonesha kwa vitendo dhima yake ya kuijenga Tanzania ya viwanda kupitia Mpango wake wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/17 hadi 2020/25.